Ungana nasi kwa kuandika email yako hapa ili upate habari mpya kupitia email yako bila usumbufu:


Showing posts sorted by relevance for query MAGAZETI. Sort by date Show all posts
Showing posts sorted by relevance for query MAGAZETI. Sort by date Show all posts

SAKATA LA KIBANDA: MAGAZETI YA MTANZANIA NA TANZANIA DAIMA HATARINI KUFUNGIWA


HATUA ya vyombo vya habari kulivalia njuga suala la kutekwa, kuteswa na kuumizwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda haiwafurahishi watendaji wa serikali.

Vyombo kadhaa vya habari yakiwemo magazeti, vimekuwa na habari, makala na maoni mfululizo kuisukuma serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi iwasake na kuwafikisha mahakamani wahusika wa tukio la Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006).

Katika habari hizo, vyombo hivyo vinaeleza kushangazwa na kitendo cha Jeshi la Polisi kushughulikia matukio mepesi haraka na kwa kutumia nguvu nyingi, huku sakata la Kibanda na lile la Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Stephen Ulimboka uchunguzi wake ukidorora.

Msukumo huo wa vyombo vya habari kuvisakama vyombo vya dola na baadhi ya vigogo serikali kuhusika na matukio hayo umepokelewa kwa mtazamo hasi.

Habari za uhakika zinasema kuwa vigogo kadhaa wameanza kuhaha kupanga mikakati ya kuvizima vyombo hivyo, hususani magazeti ya Tanzania Daima na Mtanzania ambayo yamekuwa mstari wa mbele kuandika sakata hilo.

Katika mkakati huo, tayari gazeti la Mtanzania limeandikiwa barua na Msajili wa Magazeti ambapo Kaimu Mhariri wake anatakiwa kwenda kujieleza Idara ya Habari (Maelezo) kuhusu habari iliyochapishwa Machi 20, mwaka huu.

Akithibitisha kupokea wito huo, Mhariri wa Mtanzania, Kulwa Karedia, alisema barua hiyo ina kumb. Na. IR/RN/336/57 ya Machi 21 mwaka huu, na imesainiwa na Jamal Zuberi kwa niaba ya Msajili wa Magazeti.

Alisema kuwa Kaimu Mhariri wao anajulishwa, “Madhumuni ya wito huo ni kujadili habari iliyochapishwa na gazeti lako toleo Na.7262 yenye kichwa cha Urais wa damu.”

Karedia alisema kuwa habari husika iliyoandikwa na Mtanzania ilielezea kuwa sakata la kushambuliwa kwa Kibanda limeanza kuibua tetesi na kutaka Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe ahojiwe kutokana na kauli yake.

Membe alihojiwa na kituo cha televisheni cha ITV Julai mwaka jana, katika kipindi cha Dakika 45 na kudai kuwa anao maadui 11 wakiwemo waandishi wa habari wawili ambao atawatwanga kweupe.

Hatua ya kutaka Membe ahojiwe ni kutokana na Kibanda kuumizwa ikiwa ni takribani miezi tisa tangu kauli hiyo itolewe bila kufafanua maadui zake aliwakusudia akina nani.

Hata hivyo gazeti hili lilidokezwa kuwa baadhi ya vigogo waandamizi wa serikali, CCM na maofisa kadhaa wa Usalama wa Taifa wamekuwa na vikao vya kujadili namna ya kunyamazisha magazeti hayo.

Lengo la mkakati huo ni kuhamisha mjadala ili wananchi wahangaike na mambo mengine wasahau sakata la kuteswa kwa Kibanda.


Miongoni mwa wanaohaha katika suala hili ni waziri mmoja machachari ambaye anatajwa kuusaka urais kwa nguvu akishirikiana na kigogo mwingine wa CCM.

Inadaiwa kuwa kumekuwa na vikao vya mfululizo ambapo vya mara ya mwisho vimefanyika juzi kwa siku mbili ofisini na nyumbani kwa waziri huyo jijini Dar es Salaam kujadili mkakati wao.

Miongoni mwa walioshiriki vikao hivyo yumo pia kigogo mmoja wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.

Baadhi ya mambo waliyojadili ni kuyafungia baadhi ya magazeti, hasa Tanzania Daima na Mtanzania, ambayo wamesema yanafuatilia na kuripoti sana habari za masaibu yaliyompata Kibanda.

Hata hivyo, baada ya mjadala mrefu walikubaliana kwamba ni rahisi kuanza na Mtanzania kwa sababu za kimkakati na kisiasa.


Kwa sababu zao za kimkakati walikubaliana kuanza na Mtanzania na kuliacha Tanzania Daima ambalo linamilikiwa na kiongozi wa upinzani.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya kujiridhisha kwamba mchakato wa kuvishitaki vyombo hivyo unaweza kuchukua muda mrefu na kuibua masuala mengine wasiyotaka jamii iyajue.

Vigogo hao walienda mbali zaidi wakimhusisha Ofisa Mkuu Mtendaji wa New Habari (2006), Hussein Bashe wakidai amekuwa akitumia magazeti ya Rai na Mtanzania kuelekeza yaandike masuala yanayochafua serikali, waziri mmoja na kundi lake na makundi kadhaa ndani ya CCM.

Ingawa suala la uraia wa Bashe lilishamalizika kwa Idara ya Uhamiaji kuuthibitisha, mipango ya kundi hili sasa imejielekeza katika kuibua upya suala hilo kisiasa ndani ya chama kwa kumtumia kijana machachari na bingwa wa propaganda ambaye ana wadhifa mkubwa ndani ya chama.

Taarifa zinasema suala hilo litaibuliwa ndani ya vikao vikuu vya chama vijavyo ili CCM iendelee kusisitiza haitambui uraia wake na iweke shinikizo afukuzwe uanachama.

Vile vile waliweka mkakati kuwa shinikizo hilo litapelekwa hadi kwa mwajiri wa Bashe, Rostam Aziz ili amwondoe kwenye cheo hicho au amfukuze kazi kwa sababu magazeti yake yamekuwa hayatimizi malengo asilia yaliyomsukuma kuyanunua.

Bashe ashangaa


Alipotafutwa Bashe jana kueleza kama ana taarifa za mikakati ya kikao hicho, alijibu kwa kifupi; “Sijazipata taarifa hizo ila nitazifanyia kazi.”

Bashe alikiri kupokea barua ya Msajili wa Magazeti ikiwataka wafike kujieleza Jumatatu mchana, lakini akaongeza; “Hilo suala la uraia wangu kama kweli wanaendelea nalo watakuwa wanajisumbua bure.”

Nape ang’aka

Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnuye, alipoulizwa kama anafahamu ama ameshiriki vikao hivyo vya mikakati ya kuyanyamazisha magazeti hayo, aling’aka na kusema CCM hawana matatizo na Tanzania Daima wala Mtanzania.

“Hicho kikao kinafanyikaje? Mimi ni Katibu wa Itikadi na Uenezi, huyo waziri anashughulika na wizara yake halafu huyo mtu wa Maelezo ana idara yake,” alisema.

Nape alidai hajawahi kuonana na waziri mtajwa kwa muda mrefu na kwamba hata hajui kama amerudi nchini tangu walipokutana nchini Afrika Kusini wiki kadhaa zilizopita.

“CCM kama chama hatuna matatizo na Tanzania Daima wala Mtanzania, hizo ni fitina zenu mnataka kutengeneza, vyombo hivi tunashirikiana vizuri hata niliwahi kutembelea ofisi zao baada ya kuteuliwa na hata kwenye ziara zetu mikoani tunavichukua,” alisema.

Waziri tajwa na kigogo mmoja wa Maelezo hawakupokea simu zao kutoa ufafanuzi hata walipoandikiwa ujumbe mfupi wa simu (sms) hawakujibu.

Sakata la kutekwa, kuteswa na kuumizwa vibaya kwa Kibanda linafananishwa na lile la Dk. Ulimboka kwani hadi sasa uchunguzi wa kuwasaka waliohusika unafanyika kimzaha.

Tangu alipoumizwa Dk. Ulimboka Juni 26 mwaka jana, ni mtuhumiwa mmoja pekee amefikishwa mahakamani akidaiwa kuhusika na tukio hilo ingawa inaelezwa kuwa alikuwa amerukwa na akili akajipeleka kanisani na kudai kuhusika.

Zikiwa sasa ni wiki tatu tangu kujeruhiwa kwa Kibanda, hakuna mtuhumiwa hata mmoja aliyekamatwa na vyombo vya dola kuhusiana na tukio hilo, ingawa ndani ya wiki moja Jeshi la Polisi limekamata na kumchunguza Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare kisha kumfikisha mahakamani akidaiwa kujihusisha na ugaini kwa kutumia usahidi wa video.

CHANZO: TANZANIA DAIMA

TUPE MAONI YAKO

MAALIM SIF AVITEMBELEA VYOMBO VYA HABARI VYA SERIKALI

Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Bw. Yussuf Omar Chunda (katikati) akitoa ufafanuzi juu ya shughuli zinazofanywa na Idara hiyo, wakati Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad alipofanya ziara ya kutembelea Idara hiyo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad aliangalia usanifu wa gazeti la Zanzibar leo wakati alipotembelea shirika la magazeti ya Serikali Zanzibar huko Rahaleo ikiwa ni mfululizo wa ziara zake katika taasisi za Serikali.

HABARI KAMILI:

Tume ya utangazaji Zanzibar inakusudia kufanya mazungumzo na Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko ili kujadiliana juu ya haja ya kuweka udhibiti wa kuingizwa bidhaa zinazotumia mfumo wa analog kwa vile vifaa na bidhaa hizo hazitotumika tena ifikapo mwaka 2013.

Katibu Mtendaji wa Tume hiyo Bw, Chande Omar ameeleza hayo mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad aliyefika katika ofisi za tume hiyo kuangalia maendeleo yake na changamoto inazo kabiliana nazo.

Bw. Chande amesema wakati nchi za Afrika Mashariki na Kati zikijiandaa kuachana na mfumo wa analog ifikapo Disemba mwaka huu, hakuna budi kwa bidhaa hizo kuwekewa udhibiti wa kuingia nchini, ili kuepusha mrundikano wa vifaa hivyo wakati muda wake wa matumizi utakapomalizika.

Amesema uchunguzi unaonesha kuwa licha ya vifaa hivyo kukaribia kumaliza matumizi yake, bado vimekuwa vikiingizwa kwa wingi nchini, hali inayopelekea pia uchafuzi wa mazingira.

Hata hivyo Bw. Chande amesema changamoto kubwa inayowakabili kwa sasa ni namna ya kuibadilisha jamii kuweza kutumia vifaa vya dijital kutoka analog ikizingatiwa kuwa mfumo huo unahitaji kuwa na ving’amuzi ambavyo ni ghali.

Tume hiyo pamoja na mambo mengine ina jukumu la kutoa leseni na mawimbi ya matangazo kwa vituo vyote vya radio na televisheni ambapo hadi kufikia sasa jumla ya radio 23 zimepewa leseni za kurusha matangazo pamoja na televisheni 7 zikiwemo za serikali na binafsi.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad kwa upande wake amesisitiza haja ya kuwaelimisha wafanyabiashara juu ya muda wa matumizi kwa vifaa vya analog, ili kuanza kuweka kipaumbele kwa vifaa vya dijital.

Maalim Seif ambaye pia alifanya ziara katika vyombo vya habari vya serikali vikiwemo ZBC Radio na Televisheni, Shirika la magazeti ya serikali na mitambo ya kurushia matangazo ya vituo hivyo iliyoko Bungi, Dole na Masingini pamoja na chuo cha uandishi wa habari Vuga, amesema vyombo vya habari ni muhimu kutokana na umuhimu wa taaluma hiyo katika kuwapasha habari wananchi.

Hivyo amewataka waandishi wa habari kufanya kazi kwa kujiamini na kulinda maadili ya kazi hiyo ili kuepusha migogoro katika jamii.

“Hivi sasa maadili kwa waandishi yamepotea, ni vyema kuwafunza waandishi hawa juu ya kufuata maalidili yao na waweze kuyafanyia kazi”, alisisitiza Maalim Seif wakati alipotembelea chuo cha habari Vuga kilicho chini ya mkurugenzi wake Bw. Saleh Yussuf Mnemo.

Ametoa changamoto kwa chuo kicho kutafuta eneo ili kujenga chuo kipya kinachokwenda na wakati na kuondokana na uhaba wa eneo la kufanyia sughuli zao.

Katika shirika la magazeti ya serikali, Mhariri mtendaji wa shirika hilo Bw. Abdulla Muhammed amesema shirika hilo lina mpango wa kuanzisha gazeti jengine ambalo kwa kuanzia litakuwa likichapishwa kila wiki.

Amesema hatua hiyo inakuja kutokana na gazeti moja kutokidhi haja ya kuwapasha habari wananchi, na kwamba gazeti hilo litatoa kipaumbele kwa sekta ya utalii na michezo ambazo bado hazijapewa umuhimu unaostahiki.

Bw,. Abdulla amesema shirika hilo linakabiliwa na changamoto tofauti zikiwemo baadhi ya taasisi za serikali kushindwa kulipa madeni yao magazeti na kuamua kuzuia kuzisambazia magazeti hadi hapo zinatakapojirekebisha.

Makamu wa Kwanza wa Rais aliunga mkono wazo hilo la kuzuiliwa kwa taasisi hizo kupelekewa magazeti ili kulinda mapato ya shirika.

Amelihimiza shirika hilo kuharakisha juhudi za kupata mtambo wa kuchapia magazeti ya serikali ili kuepusha usumbufu unaojitokeza ambapo kwa sasa gazeti la Zanzibar Leo linachapishwa mjini Dar es Salaam
TUPE MAONI YAKO

MISA -TAN WAPINGA KUFUNGIWA KWA GAZETI LA MWANAHALISI

TAARIFA KWA UMMA
Taasisi ya vyombo vya habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania MISA-Tanzania) inasikitika kuarifu umma wa watanzania kwamba inapinga vikali kitendo cha serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Msajili wa Magazeti Tanzania Bara kulifungia kutochapishwa kwa muda usiojulikana gazeti la MwanaHalisi kuanzia tarehe 30 Julai 2012. 

Katika taarifa iliyotolewa na serikali kupitia tangazo lake lililochapishwa kwenye magazeti mbalimbali hapa nchini na kunukuu kutolewa kwa amri hiyo kupitia gazeti la serikali (Government Notice) toleo namba 258 la tarehe 27 Julai 2012, serikali imeeleza kama ifuatavyo:

“Serikali imeamua kulifungia kutochapishwa kwa muda usiojulikana gazeti la MwanaHalisi kwa mujibu wa sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, kifungu namba 25 (i), adhabu hiyo itaanza tarehe 30 Julai 2012”

Aidha, tamko hilo la serikali limeeleza pia kuwa sababu za msingi za kulifungia gazeti hilo ni kufuatia machapisho mbalimbali ya gazeti hilo kwenye toleo Na. 302, Na. 303 pamoja na toleo Na. 304 yote yakiwa ya mwezi Julai 2012 pamoja na machapisho mengine yaliyotangulia. Serikali imeeleza kuwa machapisho hayo yamekuwa “yakichapisha habari na makala zenye kueneza na kujenga hofu kwa jamii”
 
Hata hivyo, serikali haikubainisha ni habari zipi katika machapisho hayo ambazo zinaeneza na kujenga hofu kwa jamii. Kitendo hicho cha kutobainisha habari husika kinatufanya sisi kama wanahabari na watetezi wa haki ya kupata taarifa pamoja na uhuru wa vyombo vya habari nchini na katika kanda ya kusini mwa Afrika kutoridhia maamuzi ya serikali kwani yamehusisha masuala ambayo hayakuwekwa bayana.

Ni kwa mashaka makubwa ambayo yanatokana na tamko husika la serikali kwa kutumia maneno yafuatayo:

“Kuanzia sasa serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya vyombo vya habari ambavyo kwa makusudi vitatoa taarifa za uchochezi ambazo zitahatarisha hali ya amani na utulivu uliopo nchini mwetu”
 
MISA–Tanzania inasikitishwa na kauli hiyo kwani kauli hiyo ni kudhihirisha matumizi mabaya ya sheria zilizopo katika kukandamiza uhuru wa kupata taarifa na uhuru wa vyombo vya habari kinyume na matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 18 (b) na (d) kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2005.

Haki ya kutafuta, kupata na kutoa taarifa ni haki ya msingi ya kila binadamu na imetambuliwa hivyo na Katiba ya Tanzania. Haki hii imetambuliwa pia na mikataba mbalimbali ya Kimataifa ambayo Tanzania imeiridhia bila masharti yoyote.

Kama kweli kuna taarifa za uchochezi zilizochapishwa na gazeti la MwanaHalisi na kuhatarisha amani na utulivu wa nchi, ni vyema serikali ingebainisha taarifa hizo kwenye chapisho husika na siyo kuorodhesha machapisho mbalimbali kama sababu yake ya kulifungia gazeti.

Hata hivyo, mamlaka ya serikali kufungia gazeti kupitia msajili wa magazeti ni ukiukwaji wa misingi ya haki za binadamu na matumizi makubwa ya madaraka.

Ni kwa sababu hizo kwamba Ripoti ya Haki za Binadamu iliyowahi kuandaliwa na kutolewa na Tume maalumu iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kujulikana kama Tume ya Jaji Nyalali mwaka 1992 ilibainisha sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 kuwa ni miongoni mwa sheria arobaini ambazo zinakandamiza haki za binadamu nchini. Sheria hiyo haina budi kufutwa kwenye vitabu vya sheria za nchi hii.

Kitendo cha kulifungia gazeti la MwanaHalisi kwa muda usiojulikana kinaweza kusababisha hofu kubwa kwa watetezi wa haki za binadamu na wanahabari kwa ujumla. Kitendo hicho kinafuatia kile cha kuwakamata na kuwaweka rumande (Oysterbay Polisi) wanaharakati zaidi ya kumi kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo kuandamana kufuatia mgomo wa Madaktari mnamo tarehe 9 mwezi Februari 2012. 

MISA –Tanzania inalaani vikali matumizi mabaya ya Dola katika kunyamazisha wanahabari wanapojaribu na kuthubutu kufuatilia matukio mbalimbali na kuarifu umma kuhusu yale waliyoyafanyia kazi kwa kina. Ni rai yetu kwa serikali kuwa ni vyema wabainishe taarifa mahsusi zilizopelekea maamuzi ya kufungia gazeti la MwanaHalisi ili kutuondolea hofu sisi tunaotetea haki na uhuru wa vyombo vya habari. Kuendelea kuficha taarifa husika ni kuendelea kuikanyaga Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 (ibara ya 18) kupitia kivuli cha Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 ambayo kimsingi imepitwa na wakati na haiwezi kutumika kinyume na Katiba ya nchi. 

Ni rai yetu pia kwa serikali ya Tanzania kwamba izingatie Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika yale yenye kuhamasisha utoaji haki kuliko kujikita kwenye kifungu cha 30 cha Katiba hiyo ambacho kimsingi kinaweka mipaka maalumu ya ukiukwaji wa haki za binadamu. Mipaka hiyo haionekani kuzingatiwa na serikali katika kulifungia gazeti la MwanaHalisi.
 
Kwa taarifa hii kwa umma, tunaiomba pia serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania kulifungulia gazeti la MwanaHalisi mapema iwezekanavyo na bila masharti ili kuwawezesha watanzania kuendelea kunufaika na taarifa zinazochapishwa na gazeti hilo ilmradi maadili ya uandishi wa habari yazingatiwe. Hii ni haki ya msingi kwa kila mtu na ni vyema aione ikitekelezeka.

Taarifa hii imetolewa na kusaini hapa Dar es salaam leo tarehe 31 Julai 2012.
Mohammed Tibanyendera
Mwenyekiti, MISA-TAN
TUPE MAONI YAKO

MAGAZETI YA AFRKA YAPOTOSHWA KUHUSU HABARI ZA MIKE TYSON KUBADILISHWA KUWA MWANAMKE



Tarehe 12/12/2012   iligeuka kuwa siku ya wajinga duniani badala ya April Mosi baada ya magazeti mengi ya Afrika na hasa Tanzania kuingizwa mkenge na habari ya kubuni ya Mike Tyson kubadilisha jinsia na kuwa mwanamke. 

Bahati mbaya sana ni kuwa bado watanzania wengi yakiwemo magazeti na hata baadhi ya vituo vya radio vimeendelea kuisema habari hiyo ya kupotosha kama vile ni ya kweli.


Habari hiyo hata hivyo iliandikwa mwishoni mwa mwezi November na website ya nchini Uingereza ambayo huandika habari za kubuni iitwayo NewsBiscuit.

Magazeti maarufu nchini yakiwemo Mwananchi na Jambo Leo yaliiandika habari hiyo pamoja na magazeti mengine makubwa barani Afrika kama The Standard la Zimbabwe na website ya Ghana SpyGhana.

Kwa mujibu wa BBC,NewsBiscuit ilidaiwa kuelemewa zaidi jana kutokana na wasomaji kuwa wengi kutoka Afrika.

“Tumepata wasomaji zaidi ya nusu kutoka Afrika katika siku chache zilizopita ambao tungetegemea kuwapata kwa mwezi mzima,” mwandishi wa mtandao huo John O’Farrell aliiambia BBC.

Alisema habari hiyo ilisomwa zaidi ya mara 50,000 katika siku chache tu ikiwa ni mara 20 zaidi ya kawaida.




TUPE MAONI YAKO

HII NDO MAKALA ILIYOSABABISHA "MHARIRI MTENDAJI WA TANZANIA DAIMA" AFIKISHWE MAHAKAMANI



Na Samson Mwigamba

MAKALA hii ilikuwa itoke Jumatano ya wiki iliyopita lakini kwa sababu za kiufundi ikashindikana. Imekuwa ni bahati nzuri kwamba inapotoka leo, ijibu swali la askari polisi dereva wa gari la maji ya kuwasha.

Askari huyo alimweleza Mwalimu Mkuu wa watu jinsi roho inavyomuuma pale anapowamwagia Watanzania wenzake maji hayo ya kuwasha wakati wakidai haki yao. Askari uliyeuliza na wenzako wote someni makala hii kwa utulivu. Huu ni waraka maalumu kwa askari wote wa majeshi yote vikosi vyote Tanzania Bara na Visiwani.

Kwa lugha ya wazi zaidi nazungumza na askari wa Jeshi la Polisi Tanzania, Askari wa Jeshi la Kujenga Taifa, askari wa Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM),  askari wa Jeshi la Magereza na wale wa Jeshi la Wananchi (JWTZ).
Kuwa mwanajeshi lolote kati ya hayo niliyoyataja si dhambi na si kweli kwamba kuwa mwanajeshi kunakuondolea uwezo wa kufikiri na badala yake ukawa unafikiriwa na watu wengine.

Wala haimaanishi kuwa askari kuwa kama robot ndio nidhamu bora kuliko zote duniani. La hasha! Mimi nilikataa utumwa huo!

Mwaka 1999 nilihitimu elimu ya cheti cha ufundi mchundo, yaani Full Technician Certificate (FTC) katika uhandisi wa Elektroniki na Mawasiliano ya Anga, yaani Electronics & Telecommunications Engineering kutoka Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT).

Nikiwa bado sijapata kazi ya maana, mwezi Aprili mwaka 2000 niliona tangazo la kazi ya Radio Technician katika Jeshi la Magereza. Nikatuma maombi na kuitwa kwenye usaili uliofanyika Chuo cha Maofisa wa Jeshi la Magereza Ukonga, Dar es Salaam mwezi Juni 2000.

Wote tuliofaulu usaili tulipangiwa siku ya kuripoti Chuo cha Magereza Kiwira kule Tukuyu, Mbeya.

Kufika kule nilishuhudia mambo ya ajabu. Ingawa wao hufurahia na kusema eti wanakutoa uraiani na kuwa mwanajeshi lakini baadhi ya matendo yanayofanyika wakati wa mafunzo ya jeshi ni ya kuwapumbaza askari wetu ili baadaye wakiwa kazini, watawala wawatumie watakavyo.

Nilishindwa kuvumilia kaulimbiu ya wakufunzi wa jeshi pale walipoelekeza kwamba chochote kruta (askari mpya mafunzoni) unachoambiwa lazima uitikie “ndiyo afande”. Nilishindwa kuitikia kwa mfano pale mkufunzi mmoja mwenye cheo cha koplo alipotutamkia mfululizo wa sentensi zifuatazo:
Mkufunzi: Nyinyi makruta mbona wote hamkuja na majembe?
Makruta: Ndiyo afande!
Mkufunzi: Hamkuambiwa makao makuu ya jeshi kwamba lazima mje na majembe?
Makruta: Ndiyo afande!
Mkufunzi: Kwa hiyo kwa kuwa hamkuambiwa na nyinyi hamkuyabeba?
Makruta: Ndiyo afande!
Mkufunzi:  Wote ni wapumbavu pamoja na mama zenu waliowazaa.
Makruta: Ndiyo afande!

Ni hayo pamoja na mambo mengine ya kulazimishwa kwenda kwenye kile kinachoitwa disko, ambapo pamoja na uchovu wa kutwa nzima wa kazi ngumu na nyingi bado ni lazima ukae hapo mpaka saa 4 usiku tena ukinyooshewa kidole tu na mwenzako lazima usimame na kuimbisha wimbo tena kwa tabasamu, wimbo mmoja wapo ukisema “Magereza ninavyokupenda nitakunywa sumu juu yako”, ndiyo yaliyonifanya nikakataa kazi ya jeshi baada ya wiki moja tu ya mafunzo.

Siku niliyokataa jeshi ilikuwa ni Jumatano asubuhi ambapo sikwenda mchakamchaka na wakati wenzako wanatawanyika kufanya usafi wa nje maeneo mbalimbali, mimi nilibeba begi langu na kuanza kuondoka chuoni majira ya saa moja na nusu hivi asubuhi.

Nilikamatwa na mkufunzi mmoja wa jeshi na kupelekwa pamoja na begi langu kwa Ofisa Mafunzo wa chuo. Aliponiuliza sababu nilimtajia mbili, kwanza kwamba sifurahii mambo ya jeshi na kubwa zaidi kwamba mimi ni Msabato na nimeambiwa na wenzangu kwamba hapa hakuna kwenda kusali, siku zote za juma ni kazi.

Kitu ambacho sitaweza maana Sabato takatifu lazima nipumzike! Bila kuuliza zaidi aliconclude kwa kuniambia kwamba, “Sijawahi kuona mtu anaacha kazi kwa ajili ya mambo ya dini.

”Ni dhahiri wewe ulikuja kutupeleleza na hivyo kazi yako imeisha sasa unataka kurudi. Tutakuweka rumande, tena ile ya polisi kwa wiki mbili wakati tunafanya upelelezi juu yako.”

Askari aliyenileta alianza kunivuta ili kunipeleka rumande lakini nilikataa huku nikiendelea kujieleza kwa ofisa mafunzo ili ajue kwamba sikuwa na mpango huo aliousema.

Baada ya kuelemewa na hoja zangu alinipeleka kwa makamu mkuu wa chuo ambaye yeye alitumia zaidi Biblia kunihubiri kwamba nakaidi amri ya mamlaka wakati hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu.

Jibu langu lilikuwa fupi na lenye msimamo mzito kwamba ikiwa mamlaka ya wanadamu inafika mahali inanena tofauti na Mungu, Mtume Petro ametuandikia kwamba katika hali ya namna hiyo, “Imetupasa kumtii Mungu kuliko mwanadamu”.

Na yeye alinishindwa akanipeleka kwa mkuu wa chuo na wao wote wakiwapo. Ushauri waliokuwa wakimpa mkuu wa chuo ni kwamba mimi niwekwe rumande kwanza ili wafanye upelelezi. Lakini sikuyumba katika msimamo wangu.

Nilimweleza  mkuu wa chuo kwamba mimi ni raia  na si mpelelezi. Nilizirudia rudia sababu zangu za kuacha jeshi tena kwa ujasiri mkubwa na kumhakikishia mkuu wa chuo kwamba akinipa hayo ninayoyataka niko tayari kubaki jeshini.
Hatimaye kauli ya mwisho ya mkuu wa chuo ilikuwa ni hii: “Jeshi ni wito. Tunaweza kumlazimisha huyu kijana kuwa mwanajeshi lakini baadaye ikatuletea madhara makubwa sana.” Akamalizia kwa kusema, “chukueni maelezo yake kwa maandishi kisha arudishe vifaa vya jeshi.”

Wakati naondoka nilimsikia ofisa mafunzo akitoa maelekezo kwa walio chini yake kwamba mwanafunzi mwingine wa jeshi akija kuripoti na kwenye daftari akajaza kwamba ni Msabato, msimsajili kwanza mpaka aje kwangu! Sijui kama Wasabato wameendelea kupokewa kwenye hicho chuo cha magereza lakini ninachotaka askari wote wa majeshi yetu yote na vikosi vyote, ni kwamba askari unaweza kusimama kwa miguu yako na kufikiri kwa akili yako mwenyewe!
Ndugu zangu askari, nchi imefika mahali ambapo Waingereza hupenda kupaita ‘critical point’. Ni mahali ambapo wananchi wako tayari kwa mabadiliko na watawala wako tayari kwa mapambano ili kubaki madarakani.

Katika point hii askari wetu wanakuwa na nafasi kubwa ya aidha kuwezesha mabadiliko hayo kutokea kwa wakati wanaoutaka wananchi, tena kwa amani ama kuyachelewesha (si kuyazuia) na kusababisha yatokee baadaye kidogo kuliko wananchi walivyotaka, tena baada ya kumwaga damu nyingi ya Watanzania wasio na hatia!

Napenda kurudia kwamba hakuna jeshi lolote duniani hata kama tungekusanya majeshi yote ya dunia hii na kuyaleta Tanzania hawataweza kuizuia nguvu ya umma pale inapokuwa imeamua kufanya mabadiliko.

Napenda tena kurudia kwamba si lazima askari mfanye kile ambacho wakubwa wenu wanataka na kuwaamuru kufanya. Tunaweza kusimama imara na kutetea haki za Watanzania tukiwamo na sisi askari.  Niliwahi kugoma kutii amri ya kukamatwa na kuwekwa rumande.
Lakini pia mifano ni mingi na nisingependa kuchukua mifano kutoka nchi za Ulaya kama Uingereza ambako tulishuhudia wananchi wakiandamana mitaani na askari wao hawakuwahi hata kumpiga kofi tu mwandamanaji hata mmoja.
Walipohojiwa na vyombo vya habari walisema dhahiri kwamba waandamanaji ni raia halali  wenye haki ya kufanya kile wanachokifanya kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi yao. Katiba ya Tanzania na sheria za nchi hii zinatoa haki kama zile za Uingereza. Tofauti ni utekelezaji wa matakwa hayo ya kikatiba na kisheria. Watawala wa Uingereza wako tayari  hata kung’oka madarakani ili kutekeleza matakwa ya nguvu ya umma.

Lakini wale wa Tanzania wako tayari kung’oa uhai wa raia wengi ili mradi  kuzuia nguvu ya umma inayodai  haki na   wananya hivyo kwa sababu ya hofu ya kung’oka madarakani, jambo ambalo hawataki kabisa kulisikia. Na  ndugu zangu askari napenda kuwaambia kwamba yote yanafanywa na watawala wetu kwa kuwategemea nyinyi.

Wanaminya haki zenu nyinyi wenyewe, haki za wazazi wenu, dada na ndugu zenu,  marafiki zenu, jamaa zenu na majirani zenu. Chukulia mfano rafiki zangu Mtaki na Edwin. Tumesoma wote shule ya msingi pale Magu.

Nilichaguliwa kujiunga na Mazengo Sekondari, shule kubwa na ya muda  mrefu ambayo sasa imegeuzwa kuwa chuo kikuu bila mabadiliko ya majengo.

Shule iliyokuwa na maabara nne kwa maana ya maabara ya baiolojia, kemia, fizikia na  jiografia. Ilikuwa ni sekondari ya ufundi na hakuna karakana ambayo haikuwapo.

Shule iliyokuwa na walimu wa kutosha, vyumba vya kutosha vya madarasa na vya kulala mabwenini.
Katika bweni la Ujamaa kwa mfano, nilikokuwa naishi mimi, kuna vyumba kadhaa havikuwa na watu. Darasa la Form IVA ambalo nilikuwamo lilikuwa na wanafunzi 21 tu darasani.

Na mazingira mengine mengi ambayo sitaweza kuyataja hapa ambayo yanafanya wanafunzi wa leo wa Chuo Kikuu cha Mt. John wajiulize kama kweli ile ilikuwa ni shule ambayo haina maktaba wala vitabu vya kutosha, na mengineyo mengi mnayoyafahmu.

Nikafaulu kwa kiwango cha daraja la juu lililoniwezesha kuendelea mpaka chuo kikuu na kupata kazi nzuri kwenye Umoja wa Mataiifa.

Rafiki zangu nakumbuka mlivyoamua kujiunga na Jeshi la Polisi si kwa sababu mlipenda kazi hiyo ama kwamba mlikuwa na wito wa kuwa polisi kama mnavyodanganywa kwamba jeshi ni wito.

Nakumbuka mlijiunga huku mkilalamika kwamba mnalazimika kujiunga huko kwa sababu kiwango chenu cha ufaulu hakiwapi fursa ya kazi bora zaidi ya hiyo. Lakini mimi nawafahamu vizuri. Najua uwezo wenu wa darasani. Mliathiriwa na mazingira ya hovyo ya shule mlizosoma.

Rafiki zangu nyinyi wote leo ni wakuu wa vituo vikuu vya polisi vya wilaya katika wilaya za Mbozi na Igunga.
Leo hii mimi nimeacha kazi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kushiriki vema katika mapambano ya kutafuta ukombozi wa taifa hili.

Wadogo zenu na wadogo zangu mnawajua wako katika juhudi za kutafuta maisha lakini ni magumu. Wengine walikosa kabisa nafasi ya kujiunga hata na hiyo Magu Day.

Wakaishia Bulima na Kinango, ambako hali ilikuwa mbaya zaidi. Wakafeli kabisa na leo wanahangaika hapa na pale lakini watawala wanawawekea mazingira magumu mno ya kuendesha maisha.

Na sasa chukulia nao wametambua hali yao duni inasababishwa na watawala walafi na walaghai. Wamejaribu kutumia njia za kidiplomasia kudai haki zao wanakutana na watu wanaitwa wakuu wa wilaya na mikoa.

Wanaamua kuandamana, mnashiriki kuamrisha askari walio chini yenu kuwapiga na kuwaweka rumande na hatimaye kuwafungulia kesi za kubumba!

Askari wetu igeni mfano wa askari wa Misri! Pale wananchi walipoamua kuandamana kukomesha utawala wa kidhalimu wa miaka 30 chini ya  Hosni Mubarak, askari waliwalinda badala ya kuwapiga.

Walikataa kwa sababu hata wao walikuwa wakiumizwa na Mubarak lakini zaidi ya hayo, waliokuwa wakiandamana walikuwa ni dada zao na ndugu zao na marafiki zao.

Hivi sasa nchi iko njia panda. Ugumu wa maisha umeongezeka mara nne na zaidi. Watawala hawalioni hilo wala hawajishughulishi kurekebisha hali ya mambo hususan hali ya uchumi.

Wako busy na kujiandaa kwa uchaguzi wa 2015. Mawaziri wako busy na kampeni za kuteuliwa kuwa wagombea wa urais kupitia chama tawala hapo 2015 na rais naye yuko busy kuandaa mtu wake ambaye anadhani akimrithisha jumba jeupe la pale Magogoni atasema mwacheni Ndugu Kikwete apumzike kwa amani.

Taifa limeamua kuandika katiba mpya, rais na serikali yake na chama chake wameamua kuuteka mchakato ingawa haikuwemo kwenye ilani yao ya uchaguzi ili tu waturudishie katiba ya mwaka 1977 na kuipa jina juu ya jalada KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA YA MWAKA 2014.

Natambua juhudi zinazoendelea hasa zikiongozwa na CHADEMA kujaribu kumkumbusha rais kwamba katiba iko juu yake na katiba ni mali ya wananchi na yeye anaajiriwa kwa katiba hiyo na si yeye kujiandalia katiba ili atawale kwa ulaini.

Lakini juhudi za kidiplomasia zikishindikana hapo ndipo itabidi haki ya watu idaiwe kwa maandamano na hapo askari wote tuungane na kuwa kama Misri, kwa kuwa Katiba mpya ni kwa masilahi yenu pia! Jaribuni kutafakari!
             ****MWISHO***


KUHOJIWA KIBANDA: TAARIFA YA JUKWAA LA WAHARIRI


UTANGULIZI

1. Ijumaa iliyopita, Mhariri Mtendaji wa Free Media Ltd, wazalishaji wa magazeti ya Tanzania Daima na Sayari, Absalom Kibanda alishikiliwa na kuhojiwa kwa saa kadhaa katika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi nchini.

2. Kiini cha tukio hili ni makala iliyochapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumatano, Novemba 30, 2011 ikiwa na kichwa kisemacho "Waraka maalum kwa askari wote".

3. Mwandishi wa makala hiyo, Samson Mwigamba ambaye tayari amekamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uchochezi analalamikia hulka ya polisi wa chini kutii amri hata kama amri hizo zina madhara kwa nchi na kwa mtizamo wake anasema hali hiyo inaweza kuifikisha nchi pabaya siku zijazo.

UTENDAJI WA VYOMBO VYA HABARI NCHINI

4. Umekuwa ni utamaduni kwa Msajili wa Magazeti ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) kuchukua hatua za kuvibana vyombo vya habari, hususan magazeti ambayo yamekuwa yakionekana kukiuka sheria za nchi katika uandishi wake.

5. Chini ya utaratibu huu ambao hata hivyo umekuwa ukilalamikiwa na wadau wa habari, Maelezo humwandikia barua Mhariri husika kuhusu kosa linalodaiwa kufanywa katika gazeti lake, na kutaka atoe maelezo au afike katika ofisi hizo kwa ajili ya kuhojiwa.

6. Kupitia Maelezo, hatua mbalimbali zimechukuliwa na pande husika ikiwa ni pamoja na magazeti kupewa barua za onyo, kupewa fursa ya kusahihisha taarifa husika na katika matukio machache yasiyopendeza baadhi yamewahi kufungiwa na mengine kufutwa kabisa.

7. Licha ya kasoro zake, jambo la msingi ni kwamba utaratibu wa Msajili wa Magazeti walau umekuwa ukitoa fursa watendaji wa magazeti yanayolalamikiwa kutoa maelezo ya upande wa pili lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba Uhuru wa Habari hauminywi kiasi cha kuukosesha umma taarifa muhimu za nchi na mambo yanayofanyika nchini.

KUKAMATWA KWA KIBANDA

Jukwaa la Wahariri limefuatilia kwa karibu sana tangu kukamatwa kwa Kibanda na mtindo uliotumiwa na Polisi katika kushughulikia suala hilo na kubaini yafuatayo:

8. Kwanza Makala ambayo ni chimbuko la kukamatwa kwa Mwigamba na baadaye Kibanda haikuwahi kulalamikiwa na Ofisi ya Msajili wa Magazeti kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwa taarifa nyingine nyingi, si kwa gazeti la Tanzania Daima tu, bali hata kwa magazeti mengine.

9. Kwa maana hiyo hakuna barua yoyote kutoka Maelezo ambayo iliwasilishwa Tanzania Daima ikimtaka Mhariri Mtendaji kutoa maelezo ya kimaandishi au kufika kwa msajili kujibu tuhuma za ukiukwaji wa maadili ama sheria katika makala hiyo ya Novemba 30, 2011.

10. Hakuna taarifa zozote za mtiririko wa kimatukio katika Idara ya Habari (Maelezo) au kwingineko Serikalini ambazo zinabainisha iwapo kulikuwa na onyo lolote kwa Tanzania Daima kuhusu mwenendo wake au kuhusu makala za Samson Mwigamba.

MTIZAMO NA MSIMAMO WA TEF

11. Kutokana na hali hiyo, TEF inaona kwamba kuna msukumo usio wa kawaida nyuma ya hatua ya Polisi ya kumhoji Kibanda na kwamba mwelekeo ni kuminya uhuru wa Habari na Uhuru wa kujieleza ambao umetolwa chini ya misingi ya Katiba ya nchi.

12. Msukumo huu unatokana na kuibuka ghafla kwa vyombo vya dola na zamu hii Polisi wakitumia muda mrefu katika kile walichokiita kuwa ni uchochezi, hivyo kuwafungulia wahusika KESI ZA JINAI.

13. Mashtaka haya dhidi ya Kibada na Mwigamba yanatushawishi kuamini taarifa zisizo rasmi juu ya kuwapo kwa mpango wa kuwashughulikia baadhi ya Wahariri na Waandishi wa Habari ambao wamekuwa msitari wa mbele kukosoa waziwazi miendendo ya watawala.

14. Sisi tunasema hali hii haikubaliki kwani inalenga kurejesha demokrasia ya Taifa hili nyuma zaidi ya miaka 50 iliyopita, kwa kuminya uhuru wa kujieleza na haki ya kutoa na kupata habari.

15. Mwenendo wa aina hii wa kuamu kuwashati wahariri kwa makosa ya jinai ni hatari kwa mustakabali wa nchi yetu, hasa pale vyombo vya dola vinapotumika kwa mtindo ambao umetumiwa kuwashughulikia Kibada na Mwigamba.

16. Ikumbukwe kwamba dhamira ya kupambana na wakosoaji wa utendaji Serikalini siyo tu kwamba inaathiri dhana nzima ya utawala bora wa nchi, bali inaliweka Taifa katika hatari ya kutumbukia katika uovu uliokithiri hasa pale wenye dhamana watakapofanya wapendavyo kwa kuwa tu vyombo vya habari vitakuwa vibezibwa midomo.

17. Kwa kuwa hii inaonekana kuwa dhamira rasmi ya Serikali kutumia dola kudhibiti uhuru wa habari, tunatoa mwito kwa watawala wetu kutafakari upya na ikiwezekana kuachana kabisa na dhamira hiyo.

NEVILLE MEENA,
KATIBU MKUU – TEF
KWA NIABA YA BODI YA JUKWAA LA WAHARIRI
TUPE MAONI YAKO

"SIKUENDA AFRIKA KUSINI KUJIUZA....PICHJA ZANGU ZILISAMBAA NIKIWA NIMELEWA"..AGNESS MASOGANGE


Anaweza kuwa ndo video queen hot&sexy zaidi Bongo na ingawa ameshiriki on two videos pekee anabaki kuwa Video queen mwenye jina kubwa zaidi. 

Siku za karibuni amekuwa akimake headlines on social networks pia magazeti baada ya video na picha zake chafu kusambaa on  social networks,TEENTZ imefanya nae Exclusive interview na kuongea ya moyoni kuhusu yote yanayozungumzwa kumhusu.

''Me cjui hizo picha zilisambaa vipi sababu izo picha zilikuwepo kwenye camera yangu na mimi cku hiyo nilikuwa nimelewa, i was drunk sikuwa naelewa chochote na nilikuwa south Africa kwa hiyo maswala ya kuandika habari za uongo eti nimeenda south kuuza ,me sina dhiki ya kufikia kuuza mwili wangu eti nipate pesa"na ,picha niliyopiga siyo ya uchi ile hata nikikuonesha,nilikuwa nimevaa nguo kabisa ,kuna uchi nimeonesha pale?

Na mtu kuenda South ndio ameenda kujiuza?Mimi nina biashara zangu nafanya na wanaosema hivyo hawanisaidii chochote,hakuna mtanzania anayeninunulia nguo,hayupo anayenipa pesa waongee tu''


 
Katika hatua nyingine Agness aliyashutumu baadhi ya magazeti nchini kwa kile aklichokiita wanaandika story zisizokuwa na ukweli

"Unajua sisi wadada tuna tabia ya kuoneana wivu akiona unafanya vizuri anaanza kukusemea vitu vya ajabu pembeni,Magazeti ya Bongo nayo ,wanaandika tu vitu vya kusikia pasipokuwa na uhakika na wanachokiandika nilisoma gazeti eti Wema ana mabaka,sijui Lulu amekonda ameisha,Wema alivyo mzuri vile?Lulu mwenyewe umemwona,amekonda yule?wanaandika tu imradi wauze"

Lakini pia alizungumzia uhusiano wake na mwanadada Sintah ambae awali ilitajwa kuwa wan beef lililotokana na kuvuja kwa video chafu ya Masogange.....

"Ugonvi wetu ulishaisha ,Simchukii Sintah na sitoweza kumchukia kwanza ni mkubwa kwangu yule,me niwa 1989 tu jamani,na watu hawajui me ni mpole na sipendi kugombana na watu magazeti tu wananijengea sifa mbaya"  


Kuhusu ushiriki wake katika video as video queen,Agness alifunguka kuwa hatoshiriki tena kwenye video yoyote coz mchumba wake hapendi na amemzuia.

"Nimeonekana kwenye Masogange ya Belle9 na Magube gube,sitoshiriki tena kwenye video za bongo Fleva sababu mchumba wangu amenizuia na hapendi kwanza"

 
Na hili likawa ndio neno lake kwa watanzania
"Agnes wa saivi siyo yule wa zamani nimeshabadilika jamani,me nimchumba wa mtu,nuimeshachumbiwa n soon naolewa" .alimalizia mwanadada Agness

TUPE MAONI YAKO

SKENDO ZA MAGAZETI ZAMKERA NIKKI MBISHI.........AZITUNGIA VERSE KUZIPONDA


Usicheze kabisa na Nikki Mbishi. Ni rapper ambaye anaweza kurap siku nzima bila kushika kalamu na kuandika, wanaiita mitindo huru. 
 
Apparently rapper huyu ambaye kwa sasa hupenda umuite Baba Malcom kuonesha kuwa amekua,  anakerwa na jinsi magazeti yanavyopenda kuandika skendo. So ana mashairi haya kidogo kuaddress issue hii. Sounds like a hit in the making!!!

skendo magazeti kila siku/
Nikki afumwa gesti na denti aitwaye Chiku/
eti amsahau Malcolm baada ya kufa kwa Minah/
mara akutwa akifanya ufuska na mchina/
utasikia Fetty agombea bwana na Finnah/
huku Fid Q azichapa Coco na Kalapina/
wasanii vilema wema ni manabii/
mapema wazi nasema mi sio kioo cha jamii.....!!!

Anyways, labda Nikki anatakiwa kukumbuka kuwa skendo ndo zinauza magazeti. Gazeti la udaku likijaa kuhusu kilimo kwanza,uvuvi haramu na umaskini wa nchi, halimalizi hata miezi miwili litafungwa. Usituulize kwanini!
TUPE MAONI YAKO

Haki Za Binadamu Walaani Kufungiwa MwanaHalisi


Tanzania Human Rights Defenders Coalition [THRD-Coalition]
P. O. Box 75254 Dar es Salaam, TANZANIA Telephone: +255-22-2773038/48, Fax: +255-22-
2773037, Mob: +255 783 172394 E-mail: defenderscoalition@rocketmail. com

TAMKO LA PAMOJA KUHUSU KUFUNGIWA KWA GAZETI LA KILA WIKI NA LA
UCHUNGUZI LA MWANAHALISI


Watetezi wa haki za Binadamu chini ya Mwamvuli wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDs),1 kwa ushirikiano na wadau wengine tunapinga vikali kufungiwa kwa gazeti la MwanaHalisi na Serikali mnamo tarehe 30th Julai 2012 kwa kutumia Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 Sura ya 229. Tunatambua kwamba Mwanahalisi ni gazeti la kujitegemea na la kichunguzi hapa
Tanzania.

Kwa pamoja, tumeona kuwa kufungiwa kwa Gazeti hili kunaonesha dhahiri nia ya serikali kuleta hofu na kuwanyamazisha wapigania haki za binadamu, vyombo vya habari, na watetezi wa haki za binadamu. Gazeti hili la MwanaHalisi limekuwa likitoa taarifa kwa umma kuhusu nani wahusika kwenye sakata la kutoweka na kuteswa kwa Dr Ulimboka, baada ya kuona serikali imelifumbia macho swala hili Mwahalisi limekuwa likifanya taarifa za kichunguzi ambazo zimekuwa zikitolewa kwenye mfululizo wa matoleo ya magazeti ya Mwanahalisi.

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDs) tumeguswa na swala hili na tumeona kuwa hii ni nia dhahiri ya Serikali kuvizuia vyombo vingine kutokuzungumzia masuala nyeti yenye maslahi ya umma Tunahofia kuiona Serikali inatumia sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 Sura ya 229, ambayo ni moja ya sheria mbovu na isiyo na misingi ya haki za binadamu. Sheria hii kwa miaka mingi imekuwa ikipigiwa kelele na ni sheria kandamizi, pia na ni sheria ambayo inapingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Achilia mbali kuwepo kwa Mikataba ya kimataifa na Katiba ya nchi yetu ambayo inatoa uhuru wa maoni ila bado serikali yetu imejifanya haioni ni vyema kutoa uhuru wa habari. Sheria tajwa hapo juu humpa Mamlaka mtu binafsi (Waziri) ikiwa anaona inafaa kutoa maamuzi ya kufungia Gazeti lolote kama ataona 1 The host Legal and Human Rights Centre, the Media Council of Tanzania, Media Institute of Southern Africa Tanzania chapter, and HaliHalisi representatives, Tanzania Editors Forum, Tanzania Women Lawyers Association, and Journalists for Human Rights.

ni kwa manufaa ya umma au kwa manufaa ya amani ya jamii. Sheria inamruhusu Waziri kufanya kazi za uhariri mkuu muda huo huo kufanya kazi za mlalamishi, mwendesha mashitaka, na kufanya kazi za Jaji. Hii ni kinyume na utawala wa sheria na kanuni za haki asli.Mfano katika tukio hili, misingi ya kanuni ya haki asili kam vile haki ya kusikilizwa, haki ya kukata rufaa na haki ya kusikilizwa na chombo kisichokuwa na maslahi yoyote katika shauri.

Kufungiwa kwa gazeti la Mwanahalisi hakuishii kuvunja tu uhuru wa vyombo vya habari bali pia kunavunja haki ya kupata habari kama inavyotolewa na Ibara ya 19 ya Mkataba wa Haki za kijamii na Kisiasa wa mwaka 1966 (ICCPR), Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu 1981. Kifungu cha 18 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 kinatoa uhuru wa Maoni bila kikwazo cha aina yoyote.

Kwa kitendo hiki mamilioni ya Watanzania watakuwa wamenyimwa haki ya kupata taarifa na hivyo inapunguza uwajibikaji wa viongozi wa serikali. Mtandao wa THRDs pamoja na wadau wengine tunawaomba watanzania wote na wengine wenye mapenzi mema kufanya yafuatayo;

a) Serikali

i) Kuacha kuitumia hiyo sheria kandamizi ya Magazeti ya Mwaka 1976 kwa kusudi la kunyima uhuru wa maoni na taarifa.
ii) Kuipitia upya sheria hiyo na kuifanyia marekebisho
iii) Kulifungulia Gazeti la Mwanahalisi mara moja kwa lengo la kuwapa Watanzania taarifa
iv) Viongozi na maofisa wa serikali ambao wako kwenye vyombo nyeti vya serikali kufuata maadili ya kazi, na bila kutumiwa.

b) Tasnia ya Habari

i) Kuvunja ukimya na kuonesha umoja wao katika suala hili, kwani kuumia kwa mmoja ni kuumia kwa wote.
ii) Kuendelea kutafuta na kutoa taarifa zote zenye tija na maslahi kwa umma.
iii) Kuwagundua na kuwataja waandishi wa habari wanaosaliti taaluma ya habari kwa malengo yao binafsi. Na pia kuwataka waendelee kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili na weledi wa tasnia ya habari.

c) Asasi za Kiraia.

i) Kuwa na umoja pale mtetezi wa haki za Binadamu anapopata matatizo bila ya woga.

d) Umoja wa Mataifa

Umoja wa Mataifa(UN) mawakala wake, balozi mbali mbali Tanzania na asasi zote za kikanda na za kimataifa tunawaomba kuchukua hatua katika suala hili na matukio mengine yanayowaandama watetezi wa haki za binadamu Tanzania.

e) Taasisi za kidini

Kuelewa ya kuwa Taasisi za kidini, watetezi wa haki za binadamu, wanahabari, na asasi za kiraia kwa pamoja wanapingana na rushwa, ukiukwaji wa haki na utendaji mbovu wa serikali. Hivyo basi kufungiwa kwa moja kati ya hao ni tishio na ni kinyume na misingi ya dini zote. Hivyo tunawaomba umoja wao katika hili.

f) Kwa umma

Kwa kuwa umma ndiyo watu wa kwanza kupokea taarifa za vyombo vya habari, na MwanaHalisi ikiwa moja ya gazeti la kipekee la habari za kiuchunguzi, tunawaomba kuungana nasi pamoja na wadau wengine kupinga tukio hili la kufungiwa kwa gazeti.Tuwaombe wananchi kuitaka serikali kulifungulia gazeti hili na kuifanyia mabadiliko sheria hii kandamizi.

Hili tamko la pamoja limetolewa na kusainiwa leo tarehe 2 agost, 2012 na asasi, wadau mbali mbali na watetezi wa haki za binadamu kutokana na kufungiwa kwa Gazeti la MwanaHalisi na vitisho vinavyowapata watetezi wa haki za binadamu nchini.
Imesainiwa kwa niaba ya asasi na wadau mbalimbali wanaonekana katika orodha hii na;

Dr Helen Kijo-Bisimba
Mkurugenzi Mtendaji Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu

Onesmo Olengurumwa
Mratibu Mtndao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania

ORODHA YA WADAU

1. Kituo cha sheria na Haki za Binadamu - LHRC
2. Haki Madini-Arusha
3. SAHRINGON
4. Chama cha Wanasheria wa Mazingira -LEAT
5. Chama cha Wanasheria Wanawake -TAWLA
6. Kituo cha Msaada wa Sheria Zanzibar Zan-zibar -ZLSC
7. Asasi ya Habari ya Africa kusini mwa Af-rica -MISA-Tan
8. Chama cha Wanasheria wanawake Zanzi-bar -ZAFELA
9. Jukwaaa la Jamii ya Wafugaji Tanzania -TPCF
10. Waandishi wa Habari wa Haki za Bi-nadamu-TAMWA
11. PAICODEO- Morogogoro
12. TUFAE-Songea
13. MVUHA – Shinyanga
14. CHAUMTA- Geita
15. MFUMA--Shinyanga
16. JAWAWAVI – Rukwa
17. SNDF- Shinyanga
18. Chama cha Maalbino Tanzania - TAS
19. Jukwaa la Wahariri -TEF
20. Baraza la Habari Tanzania -MCT
21. Jumuiya ya Elimu ya Haki za Binadamu na Amani- Mbeya
22. PINGOS Forum-Arusha

-------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------
Board of Directors:
Dr. Helen Kijo Bisimba, Kharous Mpatani, Martina Kabisama, Emmanuel Massawe, Annmaria
Mavenjina, Joseph Parsambei, Saed Kubenea, Hamisa Mmanga and Ernest Kimaya.
TUPE MAONI YAKO

TAMKO LA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) KUHUSU KUFUNGIWA KWA MWANAHALISI


TAMKO LA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

 KUHUSU KUFUNGIWA KWA MWANAHALISI 


Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinalaani uamuzi wa Serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kulifungia kwa muda usiojulikana gazeti la MwanaHalisi kwa kutumia mwanya wa sheria mbovu ya magazeti inayokwenda kinyume na haki za binadamu na utawala bora.

CHADEMA kinaitaka Serikali kulifungulia gazeti hilo haraka iwekanavyo na kimewasiliana na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA kuchukua hatua za kibunge kuisimamia Serikali  kurekebisha udhaifu huo ikiwa inaheshimu uhuru wa habari na inazingatia maslahi ya taifa.

CHADEMA kinatafsiri hatua hiyo ya Serikali ya kufungia gazeti la MwanaHalisi kuwa ni sawa na kufungia uhuru wa kusambaza habari, uhuru wa kupokea habari na uhuru wa kutoa maoni, hivyo tunatoa mwito kwa wananchi na wadau wote wa habari kuungana pamoja kupinga hatua hiyo, na CHADEMA kitaeleza hatua za ziada za kuchukuliwa iwapo Serikali haitasikiliza kauli za wadau wa habari juu ya suala hili.

CHADEMA kinatambua kuwa uamuzi wa Serikali kufungia gazeti hilo kwa mara nyingine tena ni kwenda kinyume na haki za binadamu, kinyume na utawala bora na ni kikwazo kwa demokrasia na maendeleo nchini.

CHADEMA kinapinga hatua ya Serikali ambayo viongozi na watendaji wake wakiwa wametajwa kama watuhumiwa katika habari zilizoandikwa na gazeti hilo imetumia mamlaka haramu ya Waziri mwenye dhamana ya sekta ya habari kugeuka mlalamikaji, mwendesha mashtaka na mfungaji huku ikipuuza taasisi za kusimamia uwajibikaji na haki.

CHADEMA ilitarajia badala ya kulifungia gazeti la MwanaHalisi ingewezesha kufanyika kwa uchunguzi huru kufuatia habari za kiuchunguzi zilizoandikwa na gazeti hilo juu ya watendaji na watumishi wa Serikali kuhusishwa na jaribio la mauji ya Dr Ulimboka Steven, kupanga njama za mauji ya viongozi wa CHADEMA na matukio mengine ambayo yenyewe ndiyo yenye mwelekeo wa kufanya wananchi wapoteze imani na vyombo vya dola hali ambayo inaweza kuhatarisha amani na mshikamano uliopo nchini.

CHADEMA kinalinganisha uamuzi huo wa Serikali uliotangazwa tarehe 30 Julai 2012 na Msajili wa Magazeti chini ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo  kuwa ni sawa  kujichukulia sheria mikononi kwa kuwa Serikali yenye kuheshimu misingi ya asili ya haki ingezingatia kwamba ikiwa chombo chochote cha habari kimedaiwa kuvunja sheria ama kukiuka maadili dhidi ya Serikali, viongozi wake ama watu binafsi mashtaka au malalamiko yangepelekwa kwa taasisi zinazohusika mathalani Baraza la Habari (MCT) au mahakama.

CHADEMA kinafahamu kuwa Serikali imeamua kulifungia kutochapishwa kwa muda usiojulikana gazeti la MwanaHalisi, kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, kifungu Na. (25) (i); hata hivyo uamuzi huo ni kinyume cha misingi ya asili ya utawala wa sheria.

CHADEMA kinaelewa kwamba zipo sheria nyingine katika nchi yetu ambazo Serikali ingeweza kuzitumia kushughulikia madai iliyoyatoa kuwa Gazeti la Mwanahalisi limeandika habari na makala za uchochezi, uhasama na uzushi kupitia mahakama lakini imeamua kwa makusudi kuendelea kutumia sheria mbaya isiyokuwa na uhalali wa kihaki (illegitimate).

CHADEMA kinakumbusha kuwa kwamba Sheria hiyo ni kati ya Sheria zilizotajwa na Tume ya kukusanya maoni juu ya mfumo wa vyama vingi (Tume ya Nyalali) kuwa ni sheria mbaya miaka 20 iliyopita kuwa na Sheria mbaya na Serikali imekuwa ikikwepa kutunga sheria mpya pamoja na wadau wa habari kuandaa miswada ya sheria ya huduma za vyombo vya habari na uhuru wa taarifa kwa nyakati mbalimbali.

CHADEMA kinatoa mwito kwa wananchi na taasisi zote za kitaifa na kimataifa kufuatilia kwa karibu tukio hili la kufungiwa kwa gazeti la MwanaHalisi na matukio mengine ya hivi karibuni kuhusu asasi za kiraia, makundi mbalimbali katika jamii ikiwemo madaktari na vyama vya siasa hususan CHADEMA yenye kuashiria kwamba Serikali inayoongozwa na CCM imeanza mkakati wa kuficha ukweli na kudhibiti mabadiliko kwa kutumia sheria kandamizi, vyombo vya dola na njia nyingine haramu.

Hivyo, ieleweke kwamba hatua hii dhidi ya Gazeti la MwanaHalisi ni mwanzo tu wa hatua zingine zaidi dhidi ya magazeti mengine na taasisi nyingine hali ambayo inahitaji wananchi na wadau wote kuunganisha nguvu za pamoja katika kuchukua hatua za haraka kuinusuru nchi na mwelekeo huo.

Imetolewa tarehe 30 Julai 2012 na:

John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
TUPE MAONI YAKO

Translate

 
Support : mpekuzi | John mpekuzi | Wataalam
Copyright © 2009. MPEKUZI - All Rights Reserved
Template designed by mpekuzi
Proudly powered by Blogger